Nimeshakata tamaa, Na nyota isiongaa,

Ndugu zangu na jamaa, Wananiona kinyaa,

Nguo zangu mechakaa, Zote rangi ya makaa,

Naona bora kupaa, Mbinguni nende kukaa.

 

Rafiki zangu wa dhati, Siku hizi hatuchati,

Wananifungia geti, Mimi siwafai eti,

Mchumbangu vayoleti, Anataka chokoleti,

Nishindwe nunua switi, Nitaweza chokoleti?

 

Nimekonda kama gonda, Na kuchoka kama punda,

Kila ofisi kienda, Mabosi wananiponda,

Kutwa zima ninashinda, bila kula hata tunda,

Japo mimi bado kinda, Mgongo umeshapinda.

 

Amini mvumilivu, Hupatwa na maumivu,

Ila twandanganywa livu, Eti ndiye hula mbivu,

Kuni hugeuzwa jivu, Kingojea kula mbivu,

Mimi na wangu werevu, Sitangoja kula mbovu.

 

Nimeshachukua kamba, Ndo nijigeuze kimba,

Ghafla sauti yatamba, Dhabiti kama ya simba,

Mdomo wangu nafumba, Kimoyomoyo naomba,

Nisamehe e Muumba, Shida ndo zimenisumba,

 

Sauti yaniambia, Yakwamba nimekosea,

Kuumba na kuumbua, Ni kazi yake Jalia,

Hapo ndo nanyenyekea, Msamaha jiombea,

Sauti yaendelea, Mema kunitabiria.

 

Nitatunga tungo bora, Kama zake walibora,

Nitalindwa na wakora, Wasiweze kunipora,

Daima tatia fora, Kama collins injera,

Taepushiwa hasira, Inayoleta hasara.

 

Mke mwema nitaoa, Ndoa isio na doa,

Wale watu hubomoa, Kwetu hawatatoboa,

Uovu tutaungoa, Kabla mizizi kutoa,

Watoto tutakopoa, Wema na waliopoa,

 

Tatangaza redioni, Kama Ali Kauleni,

Toka bara hadi pwani, Wataniweka moyoni,

Tasikizwa ofisini, Miji hata vijijini,

Afrika na marekani, Na kote ulimwenguni.

 

Kenya nitaiongoza, Vema bila kuteleza,

Nitaitoa kwa giza, Niiweke kwa mwangaza,

Mafisadi wataoza, Kiwa ndani ya gereza,

Wakenya watanipeza, zamu yangu kimaliza.

 

Yapendeza kesho yangu, Ina Mungu kesho yangu,

Ya baraka kesho yangu, Ni angavu kesho yangu,

Yavutia kesho yangu, Inangaa kesho yangu,

Yanukia kesho yangu, Hainuki kesho yangu.

 

Jicholamwewe©2017

 

Share.

About Author

Leave A Reply