“Kutafuta mke chuo kikuu ni kama kumtafuta bikira ndani ya wadi ya wazazi. Anaweza kupatikana tu iwapo Maria mzaa yesu ni miongoni mwao na usisahau Maria ni mali ya Yusufu kwa hio  kwa kifupi kama unatafuta mke naona bora ujaribu bahati yako kwenu kijijini” JLM

Nilipojiunga na chuo kikuu nilikuwa bado bikira na kwa kuwa nilidhamiria kumpa mke wangu zawadi ya ubikira usiku wa kwanza baada yetu kufunga ndoa isiokuwa na doa niliamua kuwakwepa mabinti kwa vyovyote vile. Huenda wengi walioniona kama jongoo asioweza kupanda mtungi lakini sikujali, nilijua ndani yangu kuna moto na wala sio moto wa kibatari. Ndani yangu kuna umeme utakaomfaidi mke wangu wakati ukitimia.

Haikuwa rahisi. Nakumbuka kuna siku binti fulani aliniomba nikamuone jioni moja kwa kuwa alikuwa akiumwa. Nina moyo wa kusaidia kwa hio hapakuwa na kizuizi changu kumtembelea licha ya kuwa kuingia vyumba vya wanawake wa chuo au hata kuwakaribisha chumba changu ni mwiko. Baada ya kutia na kutoa nilimwambia binti kuwa sitaweza kufika jioni hio lakini ningetafuta siku. Nikamtembelea kesho yake asubuhi na mapema nikiwa nimembebea matunda na ujumbe wa nafuu ya haraka. Nikakuta wakicheza mechi ya wawili ambayo haina refa na kijanandume ambaye alikuwa amekaribishwa baada yangu kutowahi kufika jioni. Baada ya kufanya hesabu ya haraka nikagundua alikuwa na ugonjwa ambao dawa yake ni mechi. Ndivyo walivyo wanachuo wengi.

Mara ya pili binti fulani alitaka nimpelekee kitabu chake ambacho nilikuwa nimeazima. Kutokana na jinsi alivyosisitiza nimpelekee chumbani kwake usiku wa kitu saa tatu nikitoka chuo kwenda chumbani kwangu, nikaona bora nipitie kwake nikiwa na rafiki wangu wa kiume ambaye pia alikuwa rafiki yake. Mtoto wa watu alikuwa amenivalia mavazi ya kufa mtu. Kusema la haki ule ulikuwa mtego ambao kama sio kuja na rafiki yangu, huenda singejinasua. Matukio ni mengi yanayonihusu lakini kwa leo niruhusu niangazie yanayowahusu wenzangu.

Mabinti wa vyuo ni balaa, nimeshuhudia mvulana akichomwa visu na mpenzi wake karibu afariki. Nimeshuhudia pia jamaa akifungiwa nje siku tatu na siku ya nne kurushiwa vitu vyake nje baada ya kupungukiwa na hela lakini yote tisa kumi, nimeshuhudia rafiki wangu wa karibu akifanyiwa madhila hadi karibu achizike na hapo ndipo nikaamua kuvunja ukimya.

Nina rafiki ambaye kama mimi anaamini katika kujitunza hadi siku ya ndoa hata hivyo mtu anaweza kusudia kupika sima unga ukapungua akaishia kunywa uji ama akakusudia kupika uji akaweka unga mwingi akaishia kula sima, kwa kifupi unaweza kupata usichokusudia kupata. Ajali hutokea. Mwaka jana ukielekea kuisha, rafiki yangu alinijuza kuwa kuna binti ambaye kulingana na mambo yalivyokuwa yakienda huenda akatokea kuwa ubavu wake. Akaniomba nimchunguze kisha nimfahamishe kama asonge mbele ama asitishe.

Kwa uchunguzi wa haraka nikagundua kuwa yule binti alipatikana sana kwenye mambo ya kidini na pia alikuwa na moyo wa kuwafaa watu, hata hivyo nikamuomba rafiki yangu kutopiga hatua za haraka huenda ikawa amepatana na uzuri wa mkakasi kumbe ndani kipande cha mti.

Ili kurahisisha kisa hiki naomba rafiki yangu tumpatie jina Mshamba kwa sababu kusema la haki ni mshamba wa mapenzi na kipenzi chake tumpatie jina Chausiku kutokana na kuwa yeye ni black beauty mwenye uzuri wote wa kiafrika.

Muhula ukielekea kutamatika mwaka jana mambo ya Chausiku na Mshamba yalikuwa yamenoga si haba. Mshamba akamualika Chausiku chumbani kwake kutoka jioni hadi che, hata hivyo Mshamba alinijuza kuwa hamna kilichotokea isipokuwa utalii wa mikono. Chausiku alikuwa radhi kwenda zaidi ya utalii wa mikono lakini Mshamba hakuwa tayari kupoteza ubikira. Kwa taarifa yako ilikuwa mara ya kwanza Mshamba kumkaribisha mtoto wa kike chumbani mwake na kama sikosei utalii wa mikono kama haikuwa mara ya kwanza ilikuwa ya pili.

Mwaka huu ulipoanza na muhula kuanza, safari za Chausiku ziliendelea kuongezeka katika chumba cha Mshamba, hata hivyo mshamba aliendelea kusisitiza kuwa hamna kilichotokea zaidi ya utalii wa mikono katika sehemu mbalimbali kama sio sehemu zote.

Kadri siku zilipozidi kusonga utalii wa mikono ulienda hatua nyingine, mibusu, kukandana na vitu vingine ambazo Mshamba aliniambia vinaitwa BJ (zote mshamba akizifanya kwa mara ya kwanza) kwa hio spidi hapakuwa na jingine ila Mshamba kusalimu amri. Safari yake ya karibu miongo mitatu ya kutoshiriki tendo la ndoa ikafikia tamati. Mchovya asali hawezi kuchovya mara moja, Chausiku akahamia kwa Mshamba na wote wakaadimika si haba nadhani muda mwingi walikuwa chumbani wakicheza mechi ya wawili ambayo haina refa.

Baada ya wiki kama mbili nilipatana na Mshamba na kwa ninavyomjua kuna kitu kilikuwa kikimsumbua.

“Rafiki yangu mbona unakaa stress, kwema?” nikamuuliza

“Kwema lakini Chausiku ananipatia hardtime kinoma?” akasema

“Kivipi?” nikadadisi

“Ameniambia nitafute msichana mwingine?” Mshamba alisema kwa sauti hafifu.

“Pole rafiki yangu, kuachwa ni hali ya kawaida katika ulimwengu wa sasa” nikajaribu kumliwaza

“Sijaachwa aisee”

“kama hujaachwa msichana mwingine unatafuta wa nini?”

“ili tucheze mechi watu watatu” alijibu kwa sauti nyonge

“Hata kama sijui mambo ya mechi sana najua huwa ni ya wawili tu. Huyu wa tatu atakuwa refa, linesman ama mchezaji wa akiba?”

“Chausiku ameniambia kuna kitu kinaitwa threesome which is very awesome”

Uzuri wa dunia ya sasa kuna kitu kinaiitwa google. Tulipoagana na Mshamba nilienda moja kwa moja na kutafiti kwa google na hapo ndipo nikaelewa alichokuwa akitaka Chausiku. Dunia haikosi viroja na vioja.

Baada ya muda tena Mshamba alinijuza kuwa ameambiwa atafute mwanaume kama kutafuta mwanamke imekuwa shida. Eti  mchezo ule unaweza kuwa na jike mbili na ndume moja au ndume mbili na jike moja. Kuzidisha Mshamba akaniomba niwe ndume la pili. Kwanza waswahili walisema ndume wawili hawakai zizi moja, pili kitendo kile ni kama kumkosea rafiki yangu heshima na tatu bado naamini katika kujitunza kwa hio singemsaidia Mshamba kwa vyovyote vile.

Nilimsaidia Mshamba kwa kumwambia amepatana na mbaya. Maji aliyodhani ni ya magoti yamemfika shingoni, atazama si muda mrefu. Kwa kifupi nilimwambia avunje uhusiano. Yule mtu hamfai. Hakusikia kwa kuwa alipenda na moyo badala ya kupenda na akili.

Tulipopatana tena akaniambia kuwa Chausiku alikuwa mwepesi wa kugawa. Alikuwa na marafiki wengi wa kiume lakini shida kubwa ilikuwa  hajui kusema “apana” Usiku wa kuamkia siku yetu ya kupatana Chausiku alikuwa amelala chumba cha rafiki yake wa kiume kwa kisingizio cha kuwa alikuwa amealikwa kutazama movie.

Kuna wakati tofauti kati ya mapenzi na ushenzi huwa finyu sana. Mshamba alikuwa akipika, kuosha vyombo, nyumba na hata kufua nguo zake na za Chausiku. Rafiki wake wa dhati kwa jina Shaddy caretaker wa hostel ndiye alimuita pembeni na kumshauri kuwa alikuwa akifanya mambo ya kijinga. “Ikiwa mwanamke hapiki na hajishughulishi na mambo ya usafi hafai hata kidogo”. Akaendelea kumwambia kuwa japo kibahati mtu anaweza pata mke chuo kikuu, ukweli ni kuwa kutafuta mke chuo kikuu ni kama kutafuta bikira ndani ya wadi ya wazazi, anaweza kupatikana tu iwapo Maria mzaa yesu ni miongoni mwao lakini akumbuke kuwa Maria ni mali ya Yusufu kwa hio kwa kifupi wazuri wote wamechukuliwa. Kama anataka mke bora ajaribu bahati yake kwao kijijini.

Mshamba akafura na hata kupanga kuhama hostel iliyokuwa ikisimamiwa na Shaddy kwa kujingiza kwa mambo yasiyomhusu. Shaddy akamjuza kuwa kama alikuwa anataka kuhama hapakuwa na kizuizi lakini iwapo angehama kisa na maana Chausiku angekuwa zumbukuku.

Kwa bahati nzuri kuna vitu vilifanyika jitihada za kuhama zikashindikana.

Hali ya Mshamba iliendelea kuwa mbaya. Stress zilikuwa haziishi. Kwa mfano angepitishwa stage ya nyumbani kwao akienda nyumbani na kugundua kuwa amepitishwa akiwa mbali sana. Yote haya yalikuwa yakifanyika akiwa macho sio akiwa amelala.

Kuna kipindi Mshamba alinipigia simu akiwa katika hali mbaya. Wakati huo alikuwa anaelekea kuachwa na Chausiku kwa sababu mshambulizi alikuwa amegoma kufanya mashambulizi. Alikuwa kila akiona lango analala. Anaamushwa na jitihada zote lakini kila akiamka aone lango analala kwa kasi ya ajabu. Nikamwambia kama viungo vya mwili vilikuwa zimemkataa Chausiku hakuwa na jingine ila kukubali matokea. Ikiwa una picha mbaya ya mtu akilini viungo vya mwili vitakataa kushirikiana naye haswa…..

Alifanyiwa mabaya mengi ambayo yaliwafanya wawe mara wameachana, mara wamerudiana baada ya kufanyiwa bembelezi za pilau na maji ya maembe. Mshamba na pilau na maji ya maembe ni kama sahani na kawa.

Shaddy akaanza kuugua na kufariki dunia baada ya muda mfupi.

Mshamba alipokea taarifa za kifo cha Shaddy kwa mshangao mkuu. Akampigia mtu wa kipekee ambaye alikuwa na uwezo wa kumtuliza: Chausiku.

Chausiku alipopokea ujumbe kuhusu kifo cha Shaddy simu ikakatika kama sio kukatwa. Kujaribu kumpigia tena alikuwa mteja. Usiku wa manane ndio alikuwa akituma ujumbe kuwa simu yake ilizima akaenda kuweka moto kwa rafiki yake wa kiume lakini akasisitiza kuwa hapakuwa na cha kujali kwa kuwa rafiki wake wa kiume alikuwa tayari na mpenzi wake, yeye alitandikiwa chini, wao wakalala kitandani.

Kwa kifupi siku ambayo Mshamba alimuhitaji sana Chausiku amuliwaze, Chausiku alilala chumba cha mwanaume ambacho kipo hatua chache na chumba cha Mshamba. Chumbani kulikuwa na wanawake wawili na ndume moja kwa hio kuna uwezekano wa mechi ya watatu ambayo sijui ndo inaitwa awesome ama ujinga gani.

Nilipokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa na kuamua ikitosha imetosha. Huo uhusiano kati ya Chausiku na Mshamba lazima ufike mwisho hata pilau na maji ya maembe iwepo ama isiwepo.

Zaidi ya yote nimeanzisha vuguvugu la kuwaokoa wavulana wa vyuo wasijipate pabaya kama Mshamba alivyojipata. Kwa sasa Mshamba hali yake sakarani lakini anaendelea kupata nafuu kutokana na msaada anaopata kutokana na washauri wa chuo.

 

In Memory of the late Katua, Lala pema palipo na wema swahiba

 

Share.

About Author

Leave A Reply