Tarehe kumi na mbili mei mwaka wa elfu mbili na kumi na sita, mwaka wa kwenda mbele bila kusita. Naam mwaka wa kwenda mbele bila kusita na ndio maana niliamka mapema. Mapema kuliko nilivyokuwa nikiamka katika shule ya upili ya Magumu ambapo maisha yalikuwa magumu kupita kiasi haswa kama hukuwa na pesa za kununua ‘ngumu’ ama ulikuwa nazo zikaibiwa na Jimmy. Mambo Jimmy? siku hizi uko wapi? kamiti ama mbinguni? lakini apana! ama wezi huenda mbinguni baada ya kupigwa risasi wakiiba? Ama uliokoka? na sasa uko safari ya kwenda mbinguni?…..anyway turudi kwenye kisa chetu, niliamka saa kumi na dakika sita. Niliamka kusoma. Naam kusoma. Kusoma alama za barabarani na vitu vinafanana na hivyo! Siku ya mtihani wa udereva…..

Saa kumi na mbili kasorobo nikanyemelewa na lepe la usingizi. Nikaota. Nikaota nimeitwa interviews mara si moja standard media group lakini kila wakati nikienda kuingia kufanya interviews langoni G4s hunibania. Walikuwa wakinibania kama vile lavington hubania warembo wa kiafrika chuo fulani wakijaribu kupita langoni na minisketi lakini wakawaruhusu warembo wa Korea wapite na vinyasa vya sentimeta mbili! haha sijataja chuo chochote…….Leo nikaamua liwalo na liwe lazima niingie! kukazuka mfarakano! tukazabana makofi na G4s.

Apana. hatukuzabana. Nilizabwa! hakuna haja ya kudanganya! Sijui mbona kwa ndoto ukijaribu kurusha konde haliendi. Hata hivyo nilingangana hadi wakaniruhusu kuingia ambapo baada ya kuingia ofisi ya HR nikakutana na mrembo aliyekuwa ametepwereka tepwere nikazinduka usingizini. Ndoto zina madharau wakati mwingine ila si neno!

Nikaanza kujiandaa.

Saa mbili juu ya alama nilikuwa tayari nimefika kituo cha polisi Thika. Kituo ambacho kingeamua hatma yangu; ama nitakuwa dereva ama nitabaki kuwa abiria. Saa tatu unusu mimi pamoja na mamia ya wenzangu ambao walikuwa wamekuja mtihani tukaitwa mkutano na Inspekta ambaye jina nitalibana. Akatueleza taratibu za mtihani. Mtihani ulikuwa na vitengo viwili. Maswali ya mdomo. Mdomo? Naam mdomo! Kitengo cha pili kilikuwa cha kuendesha gari.

“Dereva ana macho mangapi?” Inspekta aliuliza.

“Tatu” nikadanganya. Ama wewe umewahi kuona dereva mwenye macho matatu akiendesha matatu? Kwani driving school tunaenda kuongezewa jicho la tatu au kufundishwa kuendesha gari?

Maswali ya theory nilipita; sikupitishwa. Ama labda nilipitishwa baada ya kupita. Wote tuliobahatika kutofeli maswali tukaingizwa lori na kupelekwa eneo fulani, tukashushwa. Tukagawanywa makundi mawili. Wa gari ‘dogo na Lori. Nikaenda upande wa lori. Mateso? Tukaamrishwa kufukuza lori mbio. Wa kwanza kufikia lori anafanya mtihani. Tukawapisha akina mama kwanza. Wa kwanza akapita. Ukiona ametoka na vijikarasi jua amepita. Wa pili na watatu walitoka bila kartasi ishara ya kutopita…… Baada ya kukimbia kilomita kadhaa nikifukuza lori, zamu yangu ikafika. Nikaingia. Nikampa inspekta shikamoo.

Kama sikosei alisema mahaba badala ya marahaba. Kiswahili kigumu! Nikafunga mkanda. Nikateremsha handbrake…….. Wakati huu inspekta alikuwa akiongea kwa simu. Hivi mtu huongea kwa simu ama na simu? Bora niulize badala ya kufanya kosa baadhi ya wapenzi wa lugha wakanikashifu badala ya kunikosoa. Wanapenda sana kukashifu sijui mbona. Anyway nikangoa nanga. Wakati wote huu Inspekta alikuwa akiongea “na/kwa” simu. Alikuwa akigombanishwa na sauti ya kike; ama mke wake au ‘mchepuko’ haha wakati mwingine masikio yanaweza yakakusaliti. Nikaangalia kama kweli aliyegombanishwa na mwanamke ni inspekta. Kosa. Makofi! Naam makofi. Wala sio kupigiwa mako. Nilizabwa makofi.

“Unaangalia nini? Macho yako yanafaa kuangalia mbele na side mirror”Inspekta alifoka baada ya kunizaba makofi mawili.

“Weka gear 3!” Hasira ya kugombanishwa na mkewe au mchepuko wake bila shaka ilikuwa imeelekezwa kwangu. Nikaanza kutetemeka haswa mguu wangu wa kushoto. Sio kwa kuogopa. Apana. Nikikasirika haswa kwa sababu ya kuonewa huwa natetemeka. Mguu wa kushoto ukagoma kukanyanga clutch. Nikaweka gear ya tatu bila kukanyanga clutch. Kosa jengine! Akienda kunizaba kofi nikaachilia sterling na kukinga kofi. Lori likaingia kwa mtaro haha.

KOSA LA NANI?

Kwanza vile nilikinga hilo kofi hasira zangu zilikuwa zikinionyesha kisasi, nilikuwa tayari kumrushia konde lakini nikaona ‘kirauni’. Hata kama siheshimu mtu naheshimu taifa langu, pili nikaona kartasi yangu ambayo nilitarajia Inspekta aandike “pass” na tatu nikakumbuka korokoro si mahali pema.

Nikameza mate machungu.

Inspekta akaanza matusi. Matusi ya nguoni. Nikangoja anifukuze nje bila kartsi ya ‘pass’ kusema la haki siogopi kufeli mtihani lakini sipendi kumfeli dadangu. Dadangu ambaye amengangana kunilipia kozi hio tangu 2013. Naam nilianza 2013 lakini nikasitisha kwa sababu ya shughuli za chuo na kituo chake cha radio na gazeti. Asubuhi ya siku hio niliomba Mungu asikubali nifeli mtihani kwa vyovyote vile. Nahisi kama Mungu alimshika inspekta mkono na kuandika “pass” sasa mimi ni dereva! Halafu mtu aseme hakuna Mungu? Hata hivyo nachelewa kuamini kuwa inspekta alifaa kunizaba na kunitusi matusi ya nguoni…… Yote tisa, kumi nina uamuzi wa ama kusuka au kunyoa: uamuzi wa ama kuendesha gari au kuwa abiria.

Kaka Sam Mzalendo

 

Share.

About Author

Leave A Reply