Tumesubiri mgeni, kwa siku nyingi sikia,

ili kazi za nyumbani, apate kusaidia,

juzi kafika jioni, kwa mpigo nakwambia,

wana maajabu yaya, ila huyu kazidisha.

 

Wana maajabu yaya, ila huyu kazidisha,

Minisketi mevaliya, yenye mkato kuchosha,

Ni mhoti kama faya, maziwa ametegesha,

Huyu yaya yaya gani, au ndo kidigitali?

 

Huyu yaya yaya gani, au ndo kidigitali?

Amevalia miwani, anapimia kinduli,

kucha amezirembani, tapika vipi ugali?

Ana nyama ya ulimi, kama la kijanja toto.

 

Ana nyama ya ulimi, kama la kijanja toto,

Hashindiki kwa usemi, kama Mrisho mpoto,

Wenyeji tuso usemi, yetu tu kwake ni mato,

leo ni ya pili siku, mwenyeji utadhania,

 

Leo ni ya pili siku, mwenyeji utadhania,

Ajendake kuja huku, bado sana kungamua,

huyu dada ni ruzuku, ama ni mvunja ndoa?

Hapa mie langu jicho, tena la mwewe kumbuka.

Share.

About Author

Leave A Reply