Usiliingize guu,kwa mambo yao wakuu,
Usije ukala huu,na hasara pia juu,
Upate ujumbe huu,majuto ni mjukuu,
We’ kama hujakomaa,mapenzi na uyakome.

Haya mambo ya mapenzi,yaweza tia kichaa,
Naweza tia kitanzi,mwenzako kikuzingua,
Someni nyi’ wanafunzi,nyumae msije lia,
We’ kama hujakomaa,mapenzi na uyakome.

Hata aitwe angela,usidhani malaika,
‘Tafanya umkose mola,kwake ukiwajibika,
Ndio kwake tasema la,kilioni atacheka,
We’ kama hujakomaa,mapenzi na uyakome.

Hata aitwe Adamu, Eva usihadaike,
Gonga sepa ‘kila tamu, huenda nd’o ajendake,
Penda vitabu kalamu, masomoni ‘imarike,
We’ kama hujakomaa, mapenzi na uyakome.

‘Naweza geuka mwizi,mwenzako kumridhisha,
Ukigeuka labizi,wenzako utawachosha,
Ako wapi laazizi?kimawazo utakesha,
We’ kama hujakomaa,mapenzi na uyakome.

Moyo utayumbayumba,kiongea na wengine,
Tafikiri wakuchimba,awe mali ya mwingine,
Hapo tageuka simba,vifoni mpelekane,
We’ kama hujakomaa,mapenzi na uyakome.

Jukuani nikitoka, nilosema zingatia,
Tutavuka tukifika, naizungumzia daraja,
Hadi muda wetu ‘fika, kungojea ‘siwe hoja
We’ kama hujakomaa, mapenzi na uyakome

Share.

About Author

Leave A Reply