Wazungu husema man is to error na labda ndio maana mara nyingi watu wanapoaga dunia husifiwa hata kama walikuwa wabaya kiasi gani lakini kisa cha Moi ni tofauti.

Baada ya kifo chake watu wengi wameshindwa kufumbia macho kile ambacho wanakisema kuwa utawala wake wa kidikteta miaka ishirini aliyoongoza  huku wengine wakiamua kutrendisha hashtag ya #GoToHellMoi na #RIPMoiVictims mitandaoni.

Je ni nini kilifanya akachukiwa kiasi hicho? Hujambo na karibu tujaribu kutegua kitendawili hicho.

Moi alizaliwa Sacho, wilaya ya Baringo, Mkoa wa Bonde la Ufa, na alilelewa na mama yake Kimoi Chebii, kufuatia kuaga dunia mapema kwa baba yake.

Vitabuni, Moi alizaliwa  tarehe mbili septemba mwaka wa 1924 lakini ukweli wa mambo ni kuwa ni vigumu kubaini siku rasmi na mwaka aliozaliwa kwa kuwa enzi hizo elimu ya tarehe, mwezi, mwaka na siku ilikuwa bado haijafikia mkwafrika kikamilifu.

Baada ya kumaliza masomo katika shule ya upili ya Tambach, alijiunga na chuo cha ualimu mjini Kapsabet.

Alianza kufanya kazi kama mwalimu mwaka wa 1945 katika shule ya African Government School na mwaka mmoja baadaye akateuliwa kuwa mwalimu mkuu.

Baada ya kuhamishwa mara mbili alirudi Kapsabet mwaka 1954 akiendelea kushikilia cheo cha mwalimu mkuu, kazi ambayo aliifanya hadi mwaka 1957.

Ni katika kipindi hicho akiwa mwalimu alikutana na barafu yake ya moyo marehemu Lena Moi hata hivyo ndoa yao imadaiwa kupatwa na misukosuko Moi alipojiunga na siasa na kutengana rasmi 1974. Tangu hapo Moi hakuwahi kuoa tena.

Moi alijiunga na siasa mwaka wa 1955 na akachaguliwa kwa kiti cha wanabaraza wa mkoa wa bonde la ufa.

Mwaka wa 1960, Moi na Ronald Ngala waliunda chama cha KADU ambaycho kwa Kiswahili ni Muungano wa Demokrasia ya Waafrika wa Kenya kilichoshindana na chama cha KANU ilichoongozwa na Jomo Kenyatta.

Baada ya Kenya kupata uhuru mnamo 12 Desemba 1963, Kenyatta alimsihi Moi ya kwamba KADU na KANU ziungane pamoja kumaliza ukoloni. Kwa hiyo Kenya ikawa nchi ya chama kimoja, ikiimarishwa na muungano wa wengi Wak?k?y?-Waluo.

Moi, aliweza kupanda cheo na kuwa waziri wa mambo ya ndani mwaka 1964, hasa kwa umuhimu wake kuleta faraja za watu wa bonde la ufa na jumla KADU kwa serikali ya umoja wa Taifa.

Baadaye aliweza kupanda cheo zaidi akawa Makamu wa Rais mnamo 1967. Kama kiongozi kutoka kabila dogo, alituliza makabila haya makubwa nchini Kenya.

Lakini, Moi alipingwa na wanasiasa wa makabila makubwakubwa, hasa Wakikuyu na Waluo. Walijaribu kubadilisha katiba na kufuta kanuni iliyomfanya makamu wa rais kuchukua nafasi yake wakati rais anaaga dunia. Hata kwa uzee na afya yake Kenyatta kudhoofika, alipinga mipango hii; katiba ilibaki jinsi ilivyokuwa.

Mzee Jomo Kenyatta alipoaga dunia tarehe 22 Agosti 1978, Moi alichukua kiapo na kuwa Rais wa Kenya. Alikuwa na sifa nchini, kona zote. Alisafiri sehemu na maeneo yote Kenya, na basi wananchi wakampa faraja na hongera. Alipochukua kiapo kuwa Rais wa Kenya, alinena kwamba atafuata “nyayo” za Mzee Kenyatta, kwa maana ataendelea na sera za Kenyatta na umoja wa Harambee. Ijapokua wapinzani wake wa kisiasa, hasa kutoka makabila makubwa, walimwona Moi kama rais wa mpito tu, asiyeweza kukaa muda mrefu kwa sababu ametoka katika kabila dogo.

Agosti mosi mwaka wa  1982, kundi la askari wa jeshi la anga la Kenya, wakiongozwa na Hezekiah Ochuka, walifanya jaribio la kupindua serikali ya Moi lakini wakafeli.

Tangu hapo Moi ambaye awali alikuwa mtulivu akaja kivingine. Wote ambao walifanya jaribio hilo au hata kukisiwa kuwa walihusika kwa njia moja au nyingine walipata adhabu kali.

Katika kipondi cha uongozi wake ambao ulidumu miaka ishirini na nne, wengi wanakisiwa kuuliwa, wengi kulemazwa na wengine kuwabidi wakimbilie maisha ya nje.

Miongoni mwa watu ambao waliuliwa katika kipindi cha uongozi wake ni pomoja na aliyekuwa waziri wa mambo ya kigeni Daktari Robert Ouko ambaye aliuliwa Februari tarehe kumi na tatu 1990, Robert aliuliwa na kuchomwa moto. Robert aliuliwa siku chache baada ya kutoka ziara ya marekani ambapo inadaiwa alikutana na Rais wa marekani kipindi hicho George Bush.

Mwingine aliyeuliwa katika kipindi cha utawala wa Moi ni Bishop Alexander Kipsang Muge ambaye aliuliwa Agosti tarehe kumi na nne mwaka wa 1990., Muge alikuwa miongoni mwa viongozi wa kidini ambao walikuwa wakikosoa uongozi wa Moi.

Kabla ya kifo chake, alionywa na waziri wa leba kipindi hicho Henry Okullu   asihudhurie mkutano mkutano ambao ulikuwa umeratibiwa kufanyika Busia lakini hakusiki, alipokuwa anarudi nyumbani, aliuliwa na kile kilichosingiziwa kuwa ajali na dereva wake kufungwa kifungo cha miaka saba kwa kuendesha gari vibaya lakini akafa akiwa ametumikia kifungo cha miaka mitano. Ogopa watu aisee!

Mojawapo ya majasusi wastaafu aliambia tume ya maridhiano kuwa Askofu Alexander Kipsang Muge aliuliwa na tume ya inteliginsia na ajali ilikuwa ya kufunga watu macho.

Father Kaiser naye pia hakusazwa. Kaiser alikuwa mstari wa mbele kukosoa uongozi wa Moi. Aliwahi kukosoa uongozi wa Moi kwa kuchangia vita vya kikabila vilivyotokea mwaka wa 1991na 1992, kupinga utawala wa Moi kufunga kambi ya wakimbizi Maela, Ngong lakini pia aliwahi kuwaokoa mabinti wawili ambao walikisiwa kuwa walikuwa wamebakwa na mojawapo ya waziri katika utawala wa Moi.

Kaiser alipatikana akiwa ameuliwa Naivasha mkesha wa kuamkia Krismasi 1994.

Kiongozi wa wafanuzi chuo kikuu cha Nairobi (SONU) Titus Adungosi alihusishwa na kushawishi wanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi kufanya maandano kwa faida ya watu waliotaka kufanya mapinduzi ya serikali ya Moi.

Septemba tarehe 24 mwaka wa 1982, Titus alihukumiwa kifungo cha miaka kumi lakini akaaga dunia miezi michache kabla ya kumaliza kifungo.

Zaidi ya watu elfu tatu waliuliwa katika uwanja mdogo wa ndege wa Wagalla.

Mauaji hayo yalifanyika Februari 1984, wakati vikosi vya usalama vilipowakusanya wanaume kutoka ukoo wa Degodia kwenye harakati za kutafuta silaha haramu.

Watu hao walizuiliwa katika uwanja mdogo wa ndege wa Wagalla kwa siku kadhaa bila chakula wala maji kabla ya wengi wao kupigwa risasi walipojaribu kutoroka.

“Sitaki kuwa mahali pamoja na Moi huko mbinguni,” Bw Wamwere alisema Jumanne baada ya kifo cha Moi kutangazwa. Koigia alikuwa miongoni mwa wengi waliosota jela kwa kukosoa uongozi wa Moi. Wengine ambao walisota jela ni pamoja na Raila Odinga, Miguna Miguna, Willy Mutunga, Alamin Mazrui, Kenneth Matiba, Gitobu Imanyara, Kasisi Timothy Njoya miongoni mwa wengi wengineo.

utawala wa Rais Moi ulirudisha uchumi wa Kenya chini na Serikali yake ilikuwa na ufisadi mkubwa hadi Shirika la Fedha duniani (IMF) na Benki ya dunia (WB) walikataa kutoa mikopo kwa Kenya.

Moi ambaye alistaafu mwaka wa elfu mbili na mbili japo anakumbukwa kwa mengi mabaya, anakumbukwa kama rais ambaye aliangazia uboreshaji wa elimu bila kusahau kuwapa wanafunzi maziwa ambayo yalikuwa yakifahamika kama maziwa ya nyayo.

Alidhihirishia ulimwengu kuwa anaongozwa na demokrasia alipongatuka uongozini bila kukwamilia hadi kifo kama wanavyofanya baadhi ya viongozi wa afrika.

Katika hotuba yake ya mwisho kama Rais, Moi aliomba radhi wote aliowakosea na kusema kuwa amewasamehe wote waliomkosea.

Moi alifariki tarehe nne februari na kuzikwa tarehe kumi na mbili februari mwaka wa elfu mbili na ishirini nyumbani kwake Kapsabet.

Lala pema palipo na wema Daniel Toroitich

Share.

About Author

Leave A Reply