Profesa Ken walibora ni mojawapo ya waandishi bora kuwahi kutokea. Kando na kuwa mwandishi wa vitabu, ken alikuwa mwanahabari tajika. Huyu bwana licha ya kuzaliwa magharibi mwa Kenya, Kiswahili chake kinashinda cha wazawa wa pwani. Kando na Kiswahili Ken  Walibora aliwahi kuwafunza kizungu wazungu.

Ken Walibora alifariki kutokana na  ajali ya barabara mnamo siku ya ijumaa tarehe kumi Aprili mwaka wa elfu mbili na ishirini.

Karibu tumfahamu Swahili Shakespeare. Kipenzi cha watu aliyeliza wengi baada ya kupata ajali tarehe kumi Aprili mwaka wa elfu mbili na ishirini

Ken walibora ni kitinda mimba miongoni mwa watoto sita.

Alizaliwa tarehe sita Januari mwaka wa elfu moja mia sita tisini na nne Baraki kaunti ya Bungoma kisha wakahamia Kitale na baadae Cherangany.

Kulingana na Ken Walibora katika riwaya ya Nasikia sauti ya mama inayoelezea maisha yake, walihama Baraki baada ya kifo ndugu yake ambaye inaaminika alitiliwa sumu na mke wa ndugu wa kambo wa babake, baada ya  kaka ya Ken kufa na kuzikwa na matanga yakiwa bado hayajamalizika, Yule muuaji alipania kumua Ken Walibora ambaye alikuwa bado hajafikisha mwaka mmoja.

Mtuhumiwa anakisiwa alienda akamchukua Ken kutoka kwa dadake ambaye alikuwa amempakata, akaenda na Ken nyuma ya nyumba na dadake kumfwata ambapo alishuhudia akimlisha kitu cha ajabu. Baada ya hapo Ken afya yake ikadhoofika lakini kwa  bahati nzuri akaokolewa na wataalamu wa kuganga matatizo ya aina hio.

Alipofikisha umri wa kwenda shule mwaka wa 1971 alijiunga na shule  ya msingi  ya St. Joseph.

Ken alikuwa kisu butu darasani enzi hizo, kwa mfano alipokuwa katika darasa la pili aliwahi kuvuta mkia kwa kuibuka namba sabini na mbili katika darasa la watu sabini na wawili katika mtihani wa mwisho wa muhula wa kwanza katika shule ambayo babake alikuwa mwalimu mkuu.

Licha ya kukejeliwa na msichana mmoja aliyekuwa wakisoma naye darasa moja na ambaye alishikilia namba sita katika mtihani huo. Familia yake haikumkejeli bali ilimtia moyo mamake akimwambia;

“utafanya vyema muhula ujao, najua wewe si zumbukuku” maanake kuwa yeye si mjinga.

Licha ya kuvuta mkia, aliongoza katika somo la uchoraji.

Kipindi hicho Ken alitamani kuwa vitu viwili akija kuwa mkubwa pamoja na moja aliyochaguliwa na babake. Alipenda kuwa polisi kwa vile aliona watu waliheshimu polisi au labda kuwaogopa enzi hizo. Chaguo lake la pili lilikuwa kufanya kazi kwa redio. Babake alikuwa miongoni mwa watu wachache waliomiliki radio kijijini majirani wakilazimika kuja kwao kila jioni kusukiliza matangazo.

Chaguo la tatu na ambalo alikuwa amechaguliwa na babake ni kuwa mhandisi. Enzi hizo hakujua mhandisi ni nani lakini baada ya kufanya utafiti wa kitoto akabaini kuwa mhandisi ni fundi wa magari. Hakupenda. Hakupendezwa na pendekezo la babake la kufanya kazi ambayo ingemlazimu kuvaa msurupwenye mchafu.

Ken akiwa darasa la tano alikuwa bado hajui kusoma ndipo mamake na kisomo chake cha darasa la nne kilichomfaa kusoma Biblia ya Kiswahili na kimaragoli akaamua kufanya kile ambacho walimu walishindwa kufanya katika miaka mitano Ken alipokuwa katika mikono yao na kwa kweli alifanikiwa.

Ken akawa akimsomea mamake biblia wakati dwele zilimzidi akashindwa kusoma.

Kujua kusoma kulimfanya ajue kiulizwacho kwenye mitihani na  bila shaka akawa akijibu sahihi. Ken wa sufuri akaja vingine.

Alipofanya mtihani wa darasa la saba alikuwa wa sita katika shule yao akiwa na alama ishirini na nne kwa 36 na kujiunga na shule ya upili Teremi karibu na Kamusinga.

“Nilisomea shule tatu za upili Teremi, Suremi , O level nikasomea Olekajiado na A level nikasomea Koelel. Kutoka hapo nikawa mwalimu wa kingereza na kiswahili sekondari halafu nikajiunga na taasisi ya kenya ya utawala nikasomea maendeleo ya kijamii baadae nikawa ofisa wa probation kwa miaka minane kutoka hapo nikajiunga na KBC ambapo nilikaa kwa miaka mitatu na wakati huo huo nikajiunga na chuo kikuu ambapo nilisomea fasihi. Baadae nilijiunga na Nation media group ambapo nilisoma taarifa ya kwanza wakati Nation walifungua redio na runinga. Baada ya kufanya Nation kwa muda nilienda marekani ambapo nilisomea fasihi linganishi hadi kiwango cha PHD halafu nikafunza chuo kikuu cha Wisconsin Madison kwa takriban miaka minne halafu sasa nimerejea nchini pale pale niliopokuwa mwenzo katika kampuni ya Nation ambapo nasimamia masuala ya viwango vya lugha ya Kiswahili”

Hadi kufikwa na mauti Ken Walibora alikuwa mkurugenzi wa kituo cha masomo ya masuala ya ulimwengu na lugha pamoja na kuwa mhadhiri katika kitivo cha mahusiano ya kimataifa na diplomasia chuo kikuu cha Riara.

Chuo hicho kilitoa taafa ifuatayo kwa vyombo vya habari Ken alipoaga dunia;

Chuo kikuu cha Riara na jamii nzima ya Riara group of school imepokea kwa mshtuko kifo cha Prof. Ken Walibora kilichotokea baada ya ajali ya barabara mnamo siku ya ijumaa tarehe kumi Aprili mwaka wa elfu mbili na ishirini. Hadi kifo chake Prof. Ken Walibora alikuwa mkurugenzi wa kituo cha masomo ya masual ya ulimwengu na lugha katika chuo kikuu cha Riara. Alikuwa pia mhadhiri katika kitivo cha mahusiano ya kimataifa na diplomasia.

Mwalimu Ken, kama tulivyopenda kumuita alikuwa mwandishi tajika wa vitabu vingi katika lugha aliyoienzi ya Kiswahili. Baadhi ya kazi zake maarufu ni kama vile               Nasikia sauti ya mama, upande mwingine, kidagaa kimemwozea, ndoto ya amerika miongoni mwa nyingine nyingi. Hata hivyo, riwaya yake ya siku njema iliyochapishwa mwaka wa elfu moja mia tisa tisini ndio ilimfanya kipenzi cha wasomi wengi kote ulimwenguni na kumpa umaarufu mkubwa. Riwaya hii imetafsiriwa katika lugha nyingi na imewahi kutahiniwa katika shule za upili nchini Kenya.

Mwalimu Ken alikuwa pia mshairi mahiri. Katika ushairi, alimakinika sana katika simulizi kuhusu maisha ya jela na hatimaye aliweza kuandika kazi ya: Narrating prison experience:human right, self, society and political incarnation in Africa mwaka wa elfu mbili kumi na nne.

Atakumbukwa kama aliyekuwa mwingi wa bashasha na aliyehudumu kwa unyenyekevu. Aliwaheshimu watu wote bila kujali hadhi. Alipendwa na kuenziwa sana na wanafunzi wake pamoja na wafanyi kazi wenza. Kazi zake katika ufunzaji na utafiti zimekuwa za kusifika. Amechapisha kazi nyingi akiwa katika chuo kikuu cha Riara pamoja na kuhudumu katika makongamano, Warsha na semina nyingi za kimataifa. Jamii ya chuo kikuu cha Riara itampeza mwalimu wetu mpendwa.

Lala pema palipo na wema Prof. Ken Walibora.

Share.

About Author

Leave A Reply